Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) ndicho chombo muhimu na chenye mchango mkubwa katika kuleta maendeleo ya kiuchumi Tanzania.
Waziri Mkuu ameeleza hayo leo Desemba 22, 2020 alipokutana na Bodi mpya ya taasisi hiyo katika ukumbi wa Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam katika kikao hicho ambacho ni utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Rais Dkt. John Magufuli alipozindua Bunge la 12, jijini Dodoma, kuhusu ushirikiano kati ya serikali na TPSF.
“Sisi serikali tunapofurahi na kuwaambia Watanzania kwamba nchi yetu imeingia kwenye uchumi wa kati, hatuachi kuzungumzia namna ambavyo sekta binafsi ilivyoshiriki kikamilifu kuleta mabadiliko,” amesema Majaliwa.
“Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi hii na kwenye changamoto tutahakikisha tunazipatia ufumbuzi kwa pamoja. Serikali inaimani kubwa na Taasisi hii ya Sekta Binafsi Tanzania,” ameongeza Majaliwa.
Kwa upande wao viongozi wa taasisi hiyo wameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa ushirikiano inaowapatia ambao unawawezesha kutekeleza majukumu yao kwa urahisi na ufanisi mkubwa.
Kikao hicho pia kimehudhuriwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo, Waziri wa Viwanda na Biashara Geofrey Mwambe na watendaji wa taasisi za Serikali wanaohusika na usimamizi na uratibu wa maendeleo ya sekta binafsi.