Zoezi la utoaji chanjo ya virusi vya corona linaanza rasmi hii leo katika majimbo 16 ya nchini Ujerumani.
Watu wa kwanza kupatiwa chanjo ni wale walio na umri wa zaidi ya miaka 80, wauguzi na wafanyakazi wa hospitali ambao wako katika hatari kubwa.
Katika jimbo la Saxony mwanamke mwenye umri wa miaka 101 katika nyumba ya kutunza wazee alikuwa wa kwanza kupatiwa chanjo hiyo jana Jumamosi.
Serikali imewahimiza wananchi kupewa chanjo kwa manufaa yao na kuwalinda wengine amabpo wataalamu wamesema kiwango cha asilimia 60 hadi 70 cha chanjo ni muhimu ili kuweza kudhibiti kirusi hicho.
Nchi nyingi za Umoja wa Ulaya zinaanza rasmi zoezi hilo hii leo, wakati aina mpya kirusi kinachosambaa kwa kasi kikiripotiwa katika mataifa ya Ulaya.
Wakati huo huo, Shirika la Afya Ulimwenguni, WHO, limeonya kwamba janga hilo la sasa halitakuwa la mwisho na kwamba ni muda wa kujifunza kutoka janga la virusi vya corona.