Aina mpya ya kirusi cha corona kinachoaminika kusambaa kwa kasi, imeripotiwa kwa mara ya kwanza nchini Marekani katika mji wa Colorado na Amerika ya Kusini huku Rais mteule wa Marekani Joe Biden akiapa kuzidisha juhudi za utoaji wa chanjo.
Kirusi hicho kimegundulika kwa kijana wa miaka 20 ambaye hana historia ya kusafiri na taarifa za vyombo vya habari za ndani zinasema kuna uwezekano wa kisa kingine cha kirusi hicho.
Aina hiyo mpya ya kirusi kinachujulikana kama B.1.1.7 kimeripotiwa pia katika baadhi ya mataifa kama Canada, Italia, India na Umoja wa Falme za Kiarabu.
Chile nayo imeripoti aina hiyo mpya na kulifanya kuwa taifa la kwanza Amerika ya Kusini kubaini maambukizi yake.
Rais mteule wa Marekani Joe Biden ameonya kuhusu hali mbaya ya Covid-19 akibainisha kuwa changamoto iliyopo ni kampeni kubwa ya utoaji chanjo huko akiukosoa mpango wa mtangulizi wake Donald Trump katika usambazaji chanjo.