Mkuu wa Idara Ya Habari na Mawasilino ya Ruvu Shooting Masau Bwire ametuma salamu kwa timu za Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kuzitaka kujiandaa na kichapo, mara tu ligi hiyo itakaporejea mapema mwezi ujao.
Masau amesema kikosi chao kinachonolewa na kocha mzawa Charles Boniface Mkwasa kipo imara, na kinakitumia kipindi hiki ambacho Ligi Kuu imesimama kupisha michuano ya Fainali za CHAN, kujiandaa kwa kurekebisha makosa yaliyojitokeza katika michezo iliyopita.
Amesema dhamira yao Msimu huu ni kutwaa ubingwa, na hawawezi kufanya hivyo kama watashindwa kuziadhibu timu shiriki katika Ligi Kuu, ambayo msimu huu ina ushindani mkubwa.
“Tunatarajia kuwa imara zaidi katika michezo ya mzunguuko huu wa pili, tunaamini kocha Mkwasa anafanya kazi ya ziada katika kipindi hiki ambacho ni kizuri kwetu kujiandaa, kwa kurekebisha makosa tuliyoyafanya kwenye michezo iliyopita.”
“Tumetamka hadharani kwamba lengo letu msimu huu ni ubingwa, tukiukosa basi iwe tu Mungu hakutaka, na ikitokea tunaukosa basi watu wanatakia kuamini hivyo kwamba Ruvu Shooting walikua na hakika ya kuchukua ubingwa wa soka Tanzania Bara msimu huu 2020/21.” Amesema Masau.
Ruvu Shooting inashika nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 28, zilizotokana na ushindi katika michezo saba kupoteza michezo mitatu na kuambulia sare saba.