Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imesema inajipanga kuwa na vivutio vipya vingi vya utalii ili kumwezesha mtalii anapokuja nchini kutumia muda mrefu na kupata hamu kurudi tena kutembelea vivutio vingine.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Leila Mohamed Mussa, ambapo amebainisha kuwa Zanzibar imejipanga kikamilifu katika kuhakikisha utalii unaliingizia taifa hilo fedha nyingi za kigeni.
“Uchumi wa Zanzibar unategemea utalii kwa asilimia 28 na asilimia 80 ya fedha za kigeni zinatokanana utalii…Corona ilituathiri sana kiasi cha kukosa watalii kabisa ambao wengi walitoka Ulaya Mashariki,kwa sasa tunapata watalii wengi kutoka Ulaya Magharibi,” alibainisha.
Amesema kuwa Zanzibar inategemea utalii wa fukwe ambazo ni nzuri, lakini bado hazijaendelezwa vizuri kwaajili ya kutumika ipasavyo, na kwa sasa serikali iko katika mpango wa kuziboresha ikiwamokuunganisha vivutio vingine kama utalii wa misitu na kumwezesha mtalii kuwa na vivutio vingi nakupata muda mrefu wa kuvitembelea.
Aidha, amesema kwa sasa wanashirikiana na sekta binafsi na ametangaza fursa za watu kuwekeza katika vivutio vya kihistoria huku kipaumbele kikiwa ni kutoa ajira kwa wazawa, na kwamba kwa mwaka jana walipokea watalii 260,533.
Kuhusu Jumba la Maajabu la kihistoria la mji Mkongwe Zanzibar (Beit al-Ajaib) lililojengwa mwaka1883, ambalo ni refu zaidi lililojenga chini ya utawala wa Sultani Sayyid Bargash, amesema liliangukakwa asilimia 16.6 na sasa wako katika mpango yakinifu kwa ajili ya kulijenga upya kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la UNESCO na Serikali ya Oman.