Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli amemsamehe Mkurugenzi wa Kahama Mji, Underson Msumba kutokana na kashfa ya kununua gari la kifahari ambapo amesema amemuachia gari hilo kutokana na jinsi anavyofanya kazi vizuri na kwa kujituma akishirikiana na madiwani ambapo wamekuwa wakitekeleza miradi yenye kuwaletea maendeleo wananchi.
Rais Magufuli amesema hayo leo Alhamisi Januari 28, 2021 wakati akizungumza na wananchi wilayani Kahama.
“Mkurugenzi wa Kahama Mji unafanya kazi kubwa sana, ka kosa kale kadogo kamesamehe dhambi zako zote. Unafanya kazi sana japo unapigwa vita sana, Nimekusamehe na hilo gari nimekurudishia,” amesema Magufuli.
Rais Magufuli pia ameipandisha hadhi halmashauri ya Kahama Mji kuwa Manispaa ambapo sasa Kahama Mji itajulikana kama Manispaa ya Kahama.
“Kutokana na mahitaji yaliyopo hapa Kahama naipandisha halmashauri ya Kahama Mji kuwa Manispaa na hiyo hospitali ya Kahama iwe na hadhi ya Manispaa,” amesema Rais Magufuli.
Mkoa wa Shinyanga sasa utakuwa na Manispaa mbili (Manispaa ya Shinyanga na Manispaa ya Kahama), lakini pia kuwa na Halmashauri za Wilaya nne ambazo ni Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Shinyanga, Ushetu na Msalala.