Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ametaja mambo mawili yanayodhoofi sha michezo visiwani humo, lakini akaahidi kuwa serikali yake imejikita kurejesha heshima ya Zanzibar katika sekta ya michezo.
DK Mwinyi aliyataja mambo hayo alipokua akilihutubia taifa kupitia wahariri na waandishi wa habari Ikulu mjini Zanzibar jana Jumanne (Februari 09).
Aliyataja mambo hayo kuwa ni migogoro kwenye vyama vya michezo pamoja na kukosa udhamini kwenye michezo, kama ilivyo kwenye mataifa mengine barani Afrika na duniani kwa ujumla.
Alisema sema mambo hayo mawili yatashughulikwa ipasavyo katika kipindi cha utawala wake, ili kuondoa mkwamo katika michezo visiwani humo, na kurejesha hadhi ya Zanzibar kitaifa na kimataifa.
“Mambo mawili makubwa ambayo yanadhoofisha michezo hapa Zanzibar, moja ni migogoro kwenye vyama vya michezo. Kuna ugomvi mkubwa, mara zote wanalumbana tu hawaleti maendeleo, inakuwa ni suala la kulumbana.”
“Na malumbano haya yanatokana na vile vile na masuala ya fedha, wanagombania fedha, kuna ubadhirifu, kuna wizi, kuna rushwa. Ni mambo ambayo lazima tuyapige vita kwa nguvu zote,” alisema Dk Mwinyi na kuongeza.
“Lakini jambo la pili Zanzibar inakosa udhamini kwenye michezo. Huwezi kuendesha michezo kwa mafanikio kama hakuna udhamini. Timu kutoka Pemba kuja kucheza ligi hapa Unguja inakuwa shida, hawana fedha za kuwafikisha hapa, tukienda namna hiyo michezo haiwezi kukua.”
Dk Mwinyi alisema ni mategemeo yake kwamba baada ya kukaa na wadau changamoto zote zitaainishwa na moja baada ya nyingine zitafanyiwa kazi hatimaye Zanzibar kurejea katika kiwango chake cha michezo enzi zake ambazo hata timu za Bara zilikuwa zikienda visiwani zinajua zitapata ushindani mikubwa.