Mashabiki  na  Wanachama wa klabu ya Young Africans wametakiwa kuwa watulivu na kukiamini kikosi chao kuelekea mchezo wa mzunguuko wa 20, wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar.

Young Africans watanarajia kuwa wenyeji wa Kagera Sugar keshokutwa Jumatano, Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia mishale ya saa moja usiku.

Wito huo wa utulivu na imani kwa kikosi cha Young Africans umetolewa na, Afisa Mhamasishaji wa klabu hiyo Antonio Nugaz kupitia, ambapo amewataka kutojisikia wanyonge kufuatia matokeo ya sare ya 1-1 dhidi ya Mbeya City.

Nugaz amewasilisha ujumbe huo kupitia kwenye kurasa zake za  mitandao ya kijamii, ambapo ameandika: “Mwanachama na shabiki wa Yanga, kwanini ukajikosesha amani kwa timu kutoka sare na kuaminishwa kuwa timu haitopata matokeo na wewe unaamini hilo.”

“Kumbuka mpaka sasa tuko kileleni (namba moja) kwenye msimamo wa ligi na pia tukiwa na rekodi sahihi ya kutopoteza mchezo hata mmoja.”

“Lazima tukubaliane na matokeo ya mpira na sio kulaumu sana kana kwamba tuko nafasi ya 8 au tunaburuza mkia.”

“Tambeni mtaani, msitembee kinyonge, vimbeni mtaani na muendelee kuipa hamasa timu yetu Insha Allah kila kitu kitaenda sawa.”

“Kisha tukutane Uwanja wa Benjamin Mkapa siku ya Jumatano kwenye mchezo wetu dhidi ya Kagera Sugar saa 1:00 usiku tujitokeze kwa wingi bila kukosa.”

Wahamiaji haramu wakamatwa wakielekea Dar kutafuta kazi
Nchi za Magharibi zaitaka Myanmar kutotumia nguvu