Kikosi cha Azam FC leo Alhamis (Februari 18) kitakua na kazi kubwa ya kusaka alama tatu muhimu dhidi ya Mbeya City FC, katika mchezo wa mzunguuko wa 20 wa Ligi Kuu Tanzania Bara, utakaochezwa Uwanja wa Azam Complex Chamazi, Dar es salaam.
Azam FC watashuka dimbani leo usiku huku wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Coastal Union, kwa kufungwa mabao 2-1, kwenye uwanja wa CCM Mkwakwani.
Kocha msaidizi wa Azam FC Vivier Bahati amesema wamejiandaa kuikabili Mbeya City, na wanatumai mambo yatawanyookea baada ya dakika 90.
Amesema maandalizi ya kikosi cha Azam FC yamezingatia mapungufu yaliyojitokeza kwenye michezo miwili iliyopita dhidi ya Simba SC ambao ulimalizika kwa sare ya 2-2, kisha Coastal Union ambao ulishuhudia wakipoteza kwa mabao 2-1.
“Tumejiandaa kupambana kikamilifu tukiwa hapa Dar es salaam, kwa kushirikiana na kocha Mkuu George Lwandamina tumezingatia makosa yaliyojitokeza kwenye michezo yetu miwiwli iliopita, kwa hakika tunatumai wachezaji watakamilisha kazi ndani ya uwanja kwa dakika 90.”
“Tunawaheshimu Mbeya City kwa sababu wana kikosi kizuri, lakini hatuna budi kuamini kikosi chetu ni imara zaidi na kinaweza kupata matokeo katika uwanja wa nyumbani.” Amesema Vivier Bahati.
Katika mchezo huo Azam FC itawakosa nyota wake wawili Salum Abubakr,’Sure Boy’ ambaye ameshtua nyonga pamoja na Frank Domayo.
Domayo ambaye ni kiungo, yeye ni majera ya goti yanamsumbua na atakaa nje ya uwanja kwa muda wa mwezi mzima kabla ya kureja uwanjani.
Mbeya City inaingia kwenye mchezo wa leo Uwanja wa Azam Complex Chamazi, ikikumbuka matokeo ya sare ya 1-1 dhidi ya Young Africans, huku Azam FC itaingia uwanjani ikiwa inakumbuka ya kupoteza alama tatu dhidi ya Coastal Union.