Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Aboubakar Kunenge amesema ifikapo Alhamisi ya February 25 kituo kipya cha Mabasi yaendayo Mikoani na nje ya nchi cha Mbezi Luis kitaanza rasmi kutoa huduma na kituo cha Mabasi Ubungo kilichokuwa kikitumika awali hakitotumika tena.
RC Kunenge amesema hatua hiyo imekuja baada ya kukamilika kwa miundombinu yote muhimu ikiwemo majengo, maegesho, barabara na ofisi za kutoa huduma.
Aidha Kunenge amesema tayari Serikali imekutana na wadau wote wanaohusika wakiwemo chama cha wamiliki wa mabasi (TABOA), na wote wamejiridhisha kuwa kituo kimekamilika na kipo katika hali nzuri ya kutoa huduma hivyo wapo tayari kutoa huduma.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Sporah Liana amesema ifikapo Jumanne watafanya kikao na wafanyabiashara wote watakaokuwa wakitoa huduma ndani ya jengo na siku ya Jumatano watakutana na wamachinga, baba lishe na mama lishe, kwa ajili ya kuwekeana mikakati ya biashara.
Naye Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam, Lazaro Mambosasa amesema Jeshi la Polisi limejipanga kuhakikisha abiria wote wanaosafiri au kuingia kituoni hapo hawapati usumbufu wa aina yoyote.