Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Salama Mbarouk Khatib, amekishauri Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) kujikita katika ufanyaji wa tafiti zenye lengo kutathmini mchango wa viongozi wa wanawake waliowahi kushika nafasi za uongozi katika ngazi mbalimbali Zanzibar, ili zitumike kama mfano kwa wanawake wengine kuhamasika kujiingiza katika nafasi sizo.
Akizungumza wakati wa kikao chake na wanaume mawakala wa mabadiliko chenye lengo la kujadili na kuwakumbusha viongozi kuhusu umuhimu wa ushiriki wa wanawake katika nafasi ya uongozi chini ya TAMWA Zanzibar, Mkuu huyo wa Mkoa amesema iwapo tafiti zitafanyika zitasaidia kuionesha jamii kuhusu uwezo walionao wanawake katika uongozi.
Amesema kuwa ipo mifano mbalimbali ya wanawake waliowahi kushika nafasi za uongozi na kuzitumikia kwa mafanikio makubwa na kudai kuwa kama TAMWA Zanzibar itafanya tafiti hizo kwa kina itarejesha hamasa kwa wanawake wengine kuiga mifano hiyo.
“Nikuombeni sana TAMWA ikiwezekana tufanye utafiti, na mimi ofisi yangu ipo tayari kabisa kuungana nanyi kufanikisha hilo ili tutathimini na tutambue mchango wa wanawake waliowahi kushika nafasi za uongozi katika ngazi mbalimbali hapa Zanzibar. Tukifanyiwa tafiti hizi tunaweza kuoneshwa kwamba katika ngazi ya maamuzi ya uwaziri basi Waziri fulani alifanya vizuri zaidi,” amesema Khatib.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa mkoa amesema kuwa serikali imedhamiria kuzingatia usawa wa ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi kuanzia ngazi ya shehia hadi Taifa ili kuwaandaa na kuwajenga kuwa viongozi bora kuanzia ngazi za chini.
Amesema, “Ni kweli kwamba bado kunahitajika juhudi za kuendelea kuwajenga wanawake kuhusu dhana ya uongozi na maadili yake, ndio maana hata Serikali ya awamu ya Nane chini ya Rais, Mhe. Dk. Hussein Mwinyi imeanza kwa kuweka kipaumbele kwa wanawake katika nafasi mbalimbali, mfano mimi mwenyewe ni mwanamke na nashukuru Mhe. Rais ameniamini na kunipa nafasi hii na hii ni kuonesha ni namna gani serikali inatambua na kuthamini ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi.”
Aidha, Salama amebainisha kuwa changamoto inayochelewesha ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi ni kuwepo kwa misimamo ya kidini jambo linalotokana na kukinzana kwa tafsiri juu ya mwanamke na uongozi na kuwataka wanaume mawakala wa mabadiliko kuendelea kutoa elimu kwa viongozi wa dini zote ili kuhakikisha kunakuwa na ufahamu sawa wa wanawake katika uongozi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa wanaume mawakala wa mabadiliko, Suleiman Massoud Said alipongeza utendaji kazi wa Mkuu huyo wa Mkoa na kusema kuwa kwa kipindi chote ameendelea kuwa ni kiongozi mwanamke wa kuigwa kutokana na uchapa kazi wake.
Awali Mratibu wa TAMWA Zanzibar ofisi ya Pemba, Fat-hiya Mussa Said, alisema TAMWA ZNZ itaendelea kufanya juhudi za kuelimisha jamii kuhusu dhana ya uongozi kwa wanawake, lengo likiwa ni kuongeza idadi ya wanawake katika nafasi mbalimbali za uongozi na siasa.
Kikao hicho cha Mkuu wa Mkoa na wanaume mawakala wa mabadiliko ambao wamewezeshwa na TAMWA Zanzibar ni mwendelezo wa juhudi za Chama hicho kutetea na kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi na Siasa.