Katika jitihada za kutambua weledi, ujasiri na taaluma za Wanawake walio na mchango chanya kwenye jamii, kampuni ya Tanzania Distilleries Limited kupitia kinywaji chake cha Konyagi imebadili muonekano wa nembo ya kinywaji hicho ikiwa na picha ya mwanamke katika nembo yake iliyozoeleka kuwa na alama ya mwanaume shupavu aliyenyanyua mikono juu.
Chupa hizi maalum zina nembo yenye mwanamke aliyenyanyua mikono juu na ujumbe wa kuwatakia waTanzania heri ya siku ya Wanawake Duniani ambayo huadhimishwa kila Tarehe 8 Machi, kila mwaka.
Akizungumza na waandishi wa habari, Meneja wa bidhaa hiyo Pamela Kikuli amesema, “Konyagi ni kinywaji kinachotumiwa na watu wa jinsia zote, lakini kwa upekee, imeamua kuunga mkono wanawake wa nguvu wenye ujasiri, weledi na uwezo wa kufanya vitu vingi ambavyo vimekua vikionekana kufanyika Zaidi na wanaume kuanzia ufundi wa magari hadi uendeshaji wa kampuni kubwa.”
Pamela ameongeza kwamba Konyagi imekua ikifahamika kama kinywaji kinachopendwa Zaidi na wanaume laki ni kinywaji kinachofurahiwa na jinsia zote hivyo kumekua na umuhimu wa kipekee kutengeneza nembo maalum katika kipindi hiki cha kusherekea Siku ya Wanawake Duniani ili kutambua ujasiri wao, uwezo wao wa kusimama kama wao pamoja na utaalamu wanaotoa katika kuchangia kuendeleza jamii inayozizunguka.
“Zaidi pia tumeamua kutambua wanawake 100 wenye ujasiri, weledi na mchango kwenye jamii ya Kitanzania na kuwazawadia vitu mbali mbali ikiwemo chupa hiyo yenye nembo mpya,” amesema Kikuli.
Miongoni mwa wanawake waliotambuliwa michango yao na kupewa zawadi ni pamoja na Esther Maongezi (Mtangazaji wa TV na Redio Kipindi cha Michezo), Hellen Kazimoto (Muandaaji wa Matamasha ya Muziki) na Angellah Karashani (Mshauri wa Habari na Burudani ambao walipata fursa ya kuhudhuria kipindi cha Friday Night Live cha East Africa TV & Radio siku ya ijumaa kuzungumzia harakati zao, utaalamu wao pamoja na mchango wao katika jamii ili kuwa hamasisha Wanawake wenzao wenye ndoto waweze kuzitimiza kwa ujasiri bila uoga.
Wengine ni Leah Mollel (Muanzilishi wa Starshine TV), Mwanaidi Msuya (DJ Sweet Lady) – DJ na Rachel Pallangyo ambaye ni Refa wa Mpira wa Miguu katika ligi kuu ya Tanzania Bara (VPL), wote wakizungumzia tasnia walizopo ambazo zimekua na historia ya kuwa na wanaume zaidi lakini wao wameweza kuvunja fikra hiyo kwa kuwa vinara katika tasnia zao.
Katika kipindi hicho cha Friday Night Live kinachodhaminiwa na Konyagi, mmoja ya waalikwa hawa waliotambuliwa na Konyagi, Angellah amesema “wanaume wamekua wakiongoza vitu vingi lakini Wanawake wana uzingatiaji zaidi katika utendaji hivyo basi wakipewa kazi hua tunaitenda vizuri Kuliko wanaume. Kinachotakiwa kufanywa sio sisi kupewa fursa bali kupishwa ili tuoneshe maajabu…” alimaliza Angellah
Hii ni mara ya kwanza kwa chapa ya Konyagi kutambua mchango mkubwa wa Wanawake katika shughuli tofauti za kimaendeleo lakini kampuni hiyo imeeleza kuwa haitokuwa mara ya mwisho kwani Konyagi ina mpango wa kuendelea kuwasilisha chapa hiyo kama kinywaji kinachofurahiwa na jinsia zote.