Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema tatizo la kukatika umeme mara kwa mara nchini linamalizika leo Jumanne Machi 16, 2021 kwa sababu mitambo iliyokuwa na hitilafu imefanyiwa matengenezo.
Samia ameeleza hayo akiwa katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi mkoani Tanga ambapo amesema amezungumza na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani usiku wa kuamkia leo na amemhakikishia kwamba umeme hautakatika tena.
“Baada ya kupewa kero ya kukatika umeme nikiwa Korogwe jana usiku nimezungumza na Waziri Kalemani amenihakikishia kwamba kero ya kukatika umeme mwisho wake leo,” amesema Samia leo wakati akizungumza na wakazi wa wilayani Muheza baada ya kusimama njiani.
Amesema tatizo hilo lilijitokeza kutokana na mitambo ya kufua na kusambaza umeme kupata hitilafu na kuilazimu Tanesco kufanya matengenezo.