Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera linawasaka watuhumiwa kufuatia tukio la mwanafunzi wa darasa la nne kubakwa na kisha kuuawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani.
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Revocatus Malimi aliwaambia waandishi wa habari kuwa mtoto huyo alitoweka kuanzia Aprili 5, 2021 alipotumwa dukani na mama yake.
Alisema mtoto huyo ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kahororo ya Manispaa ya Bukoba hakurejea nyumbani kwa muda mrefu na kwamba taarifa zilieza kuwa hakufika dukani pia.
“Baada ya kusubiri kwa muda mrefu bila mtoto kurejea nyumbani, mama huyo aliamua kwenda kumuulizia dukani ambapo muuzaji alimweleza kuwa hakuwa amefika dukani hapo,” Kamanda Malimi anakaririwa.
“Akishirikiana na majirani mama huyo alimtafuta mtoto wake bila mafanikio hadi siku iliyofuata mwili wa marehemu upokutwa kwenye vichaka kando-kando mwa Ziwa Victoria eneo la Rwazi,” aliongeza.
Taarifa hiyo ya polisi imeeleza kuwa baada ya kufuatilia, waliukuta mwili wa mtoto huyo vichakani kwenye ufukwe wa Ziwa Victoria, eneo la Rwazi.
Alisema kuwa baada ya kuufanyia uchunguzi mwili wake walibaini kuwa alikuwa na majeraha katika sehemu zake za siri kutokana na kubakwa na pia alikuwa na jeraha kubwa kichwani.
Kamanda Malimi amewataka wananchi kutoa taarifa kwa siri kusaidia kupatikana kwa watu waliotekeleza ukatili huo ili wafikishwe kwenye mikono ya sheria.