Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imeukataa wosia uliokuwa ukidaiwa kuandikwa na aliyekuwa mfanyabiashara maarufu nchini marehemu Reginald Mengi pamoja na mambo mengine ikieleza kuwa haukidhi matakwa ya kisheria ili kuwa wosia halali.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji Yose Mlyambina kufuatia shauri la mirathi lililokuwa limefunguliwa na watu wanne wakiwemo ndugu wa marehemu, wakiomba kuteuliwa kuwa wasimamizi wa mirathi hiyo.
Jaji Mlyambina amefikia uamuzi huo baada ya kukubaliana na hoja za pingamizi lililowekwa na mmoja wa watoto wakubwa wa marehemu Mengi pamoja na ndugu yake marehemu Mengi, waliokuwa wakipinga uhalali wa wosia huo.
Shauri hilo la mirathi namba 39 la mwaka 2019 lilifunguliwa na Benson Benjamin Mengi, William Onesmo Mushi, Zoebu Hassuji na Sylvia Novatus Mushi wakiomba kuteuliwa kuwa wasimamizi mirathi hiyo kwa mujibu wa wosia huo.
Hata hivyo, mtoto wa Marehemu Mengi, Abdiel Reginald Mengi na ndugu wa marehemu Mengi, Benjamin Abraham Mengi, waliweka pingamizi dhidi ya wosia huo, wakipinga uhalali wake huku wakiwasilisha jumla ya sababu nne za kuupinga.
Sababu hizo ni pamoja na kwamba haukwa umepigwa mhuri na saini iliyokuwepo ilikuwa ni tofauti na saini ya kawaida ya marehemu Mengi na kwamba haukushuhudiwa na ndugu au mke wa marehemu.
Pia walikuwa wakidai kuwa marehemu hakuwa na uwezo wa kuandaa wosia kwa kuwa alikuwa na matatizo ya kiafya tangu mwaka 2016 na kwamba unaondoa katika urithi, watoto bila kuzingatia mila za Kichaga au kuhusisha ndugu.
Mahakama Kuu baada ya kusikiliza hoja za pande zote katika hukumu yake iliyosomwa juzi na Jaji Mlyambina na nakala yake kupatikana jana kwa matumizi ya umma, alikubaliana na hoja za pingamizi hilo dhidi ya wosia huo na kuikataa kuwa ni batili.
Jaji Mlyambina alikubaliana na sababu hizo za pingamizi na pamoja na mambo mengine, amesema kuwa inawanyima urithi wanaye bila kutoa sababu, na kwamba ziliiingizwa mali za mke wake mkubwa.
Kwa uamuzi huo, Jaji Mlyambina hakuwateua waombaji hao kuwa wasimamizi wa mirathi na badala yake aliwateua Abdiel na Benjamini kuwa wasimamizi wa mirathi na akaelekeza mali za marehemu zigawiwe warithi wanaostahili kwa utaratibu wa kawaida kama wa mtu ambaye hakuacha wosia.
Awali mjane wa marehemu Mengi, Jacquiline alijaribu kuingia katika shauri hilo bila mafanikio baada ya mahakama hiyo kutupilia mbali maombi yake mara tatu.