Maafisa wa polisi katika eneo la Kiminini kaunti ya Trans Nzoia nchini Kenya wanamsaka jamaa mmoja mwenye umri wa makamo aitwaye Amos Wanjala ambaye anadaiwa kuvamia makazi ya mama mkwe wake na kuchoma malazi yake.
Inaelezwa kuwa Amos Wanjala alitekeleza kitendo hicho baada ya mkewe kumtoroka.
Akiwa mwenye ghadhabu, Wanjala alivamia boma la Mercyline Wanyama Alhamisi, Mei 28,2021 majira wa saa tano usiku, alimuasha mama mkwe na kisha kuchoma malazi na baadhi ya nguo zake.
Mama huyo anasema amepoteza vitu vyenye thamani ya zaidi ya fedha za Kenya Sh 6,000 ambazo ni karibu sawa na Sh 130,000 za Kitanzania kwenye mkasa huo na hadi kwa sasa anashangaa ni nini kilichomfanya mkwe wake kumvamia.
Kulingana na taarifa ya OCPD wa Kiminini Francis Tumbo, mshukiwa anasemekana kumtishia maisha mama huyo na hivyo akikamatwa, atashtakiwa kwa uharibifu wa mali na pia kumtishia maisha mama huyo.
“Akishakamatwa, atashtakiwa kwa kosa la kuharibu mali,” amesema OCPD Tumbo.
Kwa mujibu wa taarifa za katika gazeti la The Standard la nchini Kenya, mkazi mmoja aliyetambulika kama Juma Barasa ametaka mshukiwa kuchukuliwa hatua kali za kisheria kutokana na kukiuka mila.
“Ni kinyume na ukoo wa Wabukusu kwa mtu yeyote kuwashambulia wakwe zake ama kuharibu mali yao,” Barasa alisema.
Mmoja wa majirani amesema kwamba Wanjala atapigwa faini ya mbuzi ambayo itachinjwa kwenye sherehe ya utakaso.