Katika hali isiyokuwa ya kawaida, kijana Joseph raia wa Nigeria ameweka historia ya aina yake baada ya kusoma darasa la kwanza akirudia kwa miaka 15 mfululizo bila kukata tamaa.

Kwa mujibu wa Makala maalum iliyowekwa mtandaoni na ‘ugochukwu ebuka nweke’, kijana huyo alianza shule akiwa na umri wa miaka sita, lakini maisha ya shule yamekuwa safari ndefu kwake na kujikuta ana umri wa miaka 21 katika darasa hilo la kwanza.

Mwalimu Chantal Umuhoza, alisoma na Joseph darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Gisanze. Hivi sasa yeye ni mwalimu katika shule hiyo na anamfundisha kijana huyo katika darasa lilelile.

Mwalimu Uhuhoza anasema Joseph ana tatizo la kusahau. Anasema huwa anamuweka karibu na wanafunzi wenye uelewa mzuri, anamfundisha na kuamini kuwa ameelewa; lakini baada ya muda mfupi anakuwa amesahau kila alichofundishwa.

Hata hivyo, Joseph ambaye anaamini tatizo lake la kusahau litakwisha siku moja, anasema kila anapokuwa ananyanyaswa na wanafunzi wenzake wakimuita ‘Mzee’, au baadhi ya walimu wanaomkejeli kuwa anakaribia umri wa kustaafu akiwa darasa la kwanza, yeye hakati tamaa bali anaamini ipo siku atafanikiwa na ndoto yake ya kuwa Rais itatimia.

“Ninaamini inaweza kunichukua muda mrefu, lakini mwisho wa siku nitafanikiwa na nitawafanya wazazi wangu wajivunie mafanikio yangu. Mimi nina ndoto ya kuwa Rais baada ya kuhitimu masomo yangu. Nina imani kuwa siku moja nitakuwa Rais wa nchi hii. Kwahiyo, nahakikisha nasoma kwa bidii ili nikamilishe ndoto yangu. Ninaamini kuwa Mwenyezi Mungu atanisaidia kukamilisha ndoto yangu,” amesema Joseph.

Aliyesema ‘Mama ni nguzo ya maisha ya jamii’, achongewe sanamu ikae juu ya paa la Ikulu. Dunia ikikukataa, mama atakuwa nguzo ya kuegemea.

Mama mzazi wa Joseph, anasema kuwa ni mwanaye wa pili kumzaa na anaumia anapoona wenzake aliosoma nao darasa hilo la kwanza wameshafikia hatua ya kupata kazi na wengine ni waheshimiwa kwenye ulingo wa siasa.

“Hivi sasa ana umri wa miaka 21, lakini amerudia darasa hilo moja mara 15, yaani kwa miaka 15. Waliosoma naye wengine hivi sasa ni Mameya wa majiji na waheshimiwa. Mwanangu ana tatizo la kiakili linalomfanya asahau haraka. Huko shuleni, walimu wanasema ananyanyaswa na baadhi ya wanafunzi wakorofi wanaodai ana kichwa kikubwa lakini hakina kitu. Lakini yeye mwenyewe ananipa moyo kuwa tuendelee kupambana huenda siku moja akafanikiwa. Ninafurahi ambavyo hakati tamaa. Siku zote ananiambia siku atakapoweza kufaulu atakuwa Rais wa nchi hii,” Mama Joseph anaeleza.

Hata hivyo, mama huyo anasema sio tu kwenye masuala ya shuleni, bali Joseph ana tatizo la kusahau hata katika shughuli za nyumbani. Anasema mara nyingi hujikuta katika mgogoro na wafanyabiashara pale anapomtuma dukani.

“Ninaweza kumtuma beseni lakini yeye akaenda kununua shuka, ninaporudisha huwa kunakuwa na ugomvi. Lakini kwa sasa wafanyabiashara wengi wa hapa wameshamzoea, wanaona ni kawaida anaposahau,” anasimulia.

Mama anasema mwanaye anaamini siku moja atakuwa Rais, na yeye anamuombea aweze kukamilisha safari yake ya shule bila kukata tamaa.

Mama Joseph anasema mwanaye anamtia moyo zaidi kwa jinsi alivyo na kiu ya kujifunza na kutokata tamaa.

“Kuna kitu cha kipekee sana ambacho mwanangu anacho, anajiamini na anaweka bidii sana katika kujifunza. Hawezi kuchelewa kuingia darasani hata mara moja, na huwezi kumzuia kwenda shule. Uwezo wake wa kuingia darasani uko katika kiwango cha juu sana, anapenda kwenda darasani hata kama wenzake wanamnyanyasa,” amesema Mama Joseph.

Je, wewe umekata tamaa kwenye lipi? Fuata nyayo za Joseph na muombe Mwenyezi Mungu, hakuna kinachoshindikana.

Bumbuli ajibu hoja za Manara
CAG awasilisha ripoti ya fedha zilizochukuliwa Benki Kuu, Januari - Machi