Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limesikitishwa na linalaani kitendo cha Msemaji wa Klabu ya Simba, Haji Manara kumdhalilisha Mwandishi wa Habari wa Radio Clouds FM, Prisca Kishamba.
Udhalilishaji huo ulioambatana na maneno ya kashfa dhidi ya Prisca, ulifanywa na Msemaji huyo wa Simba kwenye mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika Juni 30, 2021, katika Hoteli ya Serena, Dar es Salaam.
Mkutano huo pamoja na mambo mengine, ulizungumzia mchezo wa Ligi Kuu ya Bara baina ya timu ambazo ni watani wa jadi; Simba na Yanga.
Kauli za vitisho vya Manara ni mwendelezo wa tabia na mwenendo wake dhidi ya Waandishi wa Habari ambao wamekuwa wakiripoti habari za Klabu ya Simba kwa maslahi mapana ya umma na Sekta ya michezo kwa ujumla.
Tukio la Juni 30 dhidi ya Prisca na Waandishi wa Habari wengine walipokuwa wakiuliza maswali kwenye mkutano huo, linafikirisha na linatufanya tutafakari ikiwa ni sahihi kwa vyombo vya habari kuendelea kuripoti habari zinazitolewa na Klabu ya Simba kupitia kwa Msemaji wake huyo.
Kimsingi vitendo vya aina hii vinavyofanywa na Haji Manara kwa Waandishi wa Habari siyo vya kiungwana na havivumiliki hata kidogo.
Wakati waandishi wa habari wanapokuwa kazini mara zote tumekuwa tukiwahimiza kufuata maadili ya kazi zao, vivyo hivyo kwa watoa habari wanapaswa kuwa waungwana hata pale wasipotaka kuyasikia maswali wasiyoyapenda.
Kwa tamko hili, tunamtaka Manara aache mara moja tabia ya kutumia mikutano ya Klabu ya Simba kwa Waandishi wa Habari na hata mitandao ya kijamii kuwadhalilisha wanahabari.