Mgombea aliyeenguliwa katika mchujo wa awali wa kugombea urais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Ally Salehe amesema ana mpango wa kuchangisha fedha ili kukusanya Shilingi Milioni 25 za kuendesha kesi hiyo.
Salehe alifungua kesi Mahakama Kuu kupinga mchakato wa uchaguzi huo wa TFF uliopangwa kufanyika Agosti 8 mwaka huu kutoitambua Zanzibar, kesi namba 98 na kesi ndogo ya kusitisha mchakato wa uchaguzi huo ambazo zote zitasikilizwa kwa mara nyingine Ijumaa hii.
Wakati wadau wakisubiri hatma ya uchaguzi huo, Salehe ameanzisha kampeni ya kukusanya Sh 25 Milioni ambazo alisema ni za matumizi ya kuendesha kesi hiyo.
“Hii kesi siyo yangu kama Salehe, nipo kwa ajili ya kutetea maslahi ya umma, hivyo si vibaya wadau wakashirikiana nami katika kuwalipa mawakili na huduma nyingine,” alisema.
Alisema hadi jana alikuwa amechangiwa zaidi ya Sh 1.5 milioni hivyo anaendelea kupokea michango mingine kutoka kwa wadau.
Chanzo: Mwanaspoti