Kikosi cha Coastal Union kimejiandaa ‘KUPIGA PANAPOUMA’, watakapokutana na Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, mwishoni mwa juma hili Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Coastal Union wamejipanga kufanya hivyo, kufuatia Simba SC kupoteza mchezo wake dhidi ya Young Africans juzi Jumamosi (Julai 03), huku ikikabiliwa na mchezo mwingine dhidi ya KMC FC keshokutwa Jumatano (Julai 07).
Kocha Mkuu wa timu hiyo yenye maskani yake makuu jijini Tanga Juma Mgunda amesema maandalizi ya kuelekea mchezo wao dhidi ya Simba SC utakaochezwa Julai 11, yanakwenda vizuri, na wanaamini watapata matokeo chanya.
Mgunda amesema kuwa ushindani ni mkubwa na kila timu inahitaji ushindi, lakini hitaji la alama tatu kwa kikosi chake ni kubwa sana, hivyo watahakikisha wanaibamiza Simba SC, kwa ‘KUPIGA PANAPOUMA’.
“Vijana wapo vizuri kwani kila mchezaji anajua kwamba tunahitaji ushindi na mechi zetu ambazo zimebaki ni lazima tupambane hivyo mashabiki waendelee kutupa sapoti.
“Kila mmoja anahitaji kuona kwamba tunarejesha hali ya kujiamini na hilo linawezekana hasa ukizingatia kwamba kila timu inahitaji kupata pointi tatu,” amesema Mgunda.
Mchezo wa mzunguumo wa kwanza shisi ya Simba SC, Mgunda alishuhudia kikosi chake kikilambishwa shubiri kwa kubanjuliwa 7-0 jijini Arusha katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.