FC Barcelona huenda ikamuachia Nahodha na Mshambuliaji wake kutoka nchini Argentina Lionel Messi kuondoka klabuni hapo kama mchezaji huru, kufuatia mkataba wake kufikia kikomo mwezi uliopita.
Licha ya FC Barceleona kutarajia kufanya hivyo, bado Messi mwenye umri wa miaka 34 ana nafasi ya kusaini mkataba mpya ambao utamuwezesha kusalia klabuni hapo kwa miaka mingine isiopungua miwili.
Mpango wa kusaini mkataba mpya ama kuondoka kwa Mshambuliaji huyo, utafahamika atakaporejea Hispania, baada ya fainali za Copa America zinazoendelea nchini Brazil.
Sintofahamu kuhusu Lionel Messi, imeanza kumletea matatizo makubwa rais Joan Laporta, ambaye anatazamwa kama mtu wa mwisho kumshawishi mshambuliaji huyo kusaini mkataba mpya, huku FC Barcelona ikiwa na deni la Pauni Bilioni 1.
Mshindi huyo mara sita wa Ballon d’Or ambaye alikuwa akivuna Pauni milioni 122 (Sh 393 Bilioni) kila msimu kwenye mkataba wake uliomalizika, ameifanya Barca kuwa kwenye wakati mgumu wa kutafuta namna ya kumfanya aendelee kubaki kwenye timu yao baada ya dirisha hili la majira ya kiangazi kupita.
Hata hivyo mabosi wa timu hiyo wanahitaji kuwaondoa wachezaji wawili wenye mishahara mikubwa kwenye kikosi hicho bure kabisa ili kuokoa pesa zitazomfanya Messi abakizwe.
Mastaa wawili waliopo kwenye hatari ya kutemwa ni beki wa kati Samuel Umtiti na kiungo wa kati, Miralem Pjanic, huku wote hao wakiripotiwa kutokuwapo kwenye mipango ya kocha Ronald Koeman katika kuelekea msimu mpya wa Laliga.