Baba wa Nahodha na Mshambuliaji wa Timu ya Taifa ya Tanzania *Taifa Stars* Mbwana Samatta, amejitosa kwenye mjadala wa mpambamo wa Kariakoo Dabi uliochezwa Jumamosi (Julai 03), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Ally Pazi Samatta, baba wa Mshambuliaji huyo anaekipiga kwenye ligi ya Uturuki amesema kama Simba ingeishinda Young Africans, Kiungo Mshambuliaji kutoka Ghana Bernard Morrison, angetamba maradufu.
Mzee huyo amesema akili ya kazi ya Morrison imekomaa licha ya kwamba ni mchezaji aliyeongoza kwa kuzomewa lakini hakujali zaidi ya kutimiza majukumu aliyopangiwa na kocha wake Didier Gomes.
“Ndani ya kikosi mkiwa na wachezaji saba kama Morrison timu hiyo inakuwa tishio, anajua yeye ni nani katika majukumu yake, ndicho alichokifanya kwenye mchezo wa watani, Young Africans ndio ilikuwa na presha kipindi cha pili kutokana na Simba kufika langoni kwao mara kwa mara, huku Morrison akitumia akili kubwa kutengeneza faulo nyingi,”
Amesema bahati mbaya Simba, ilipoteza mchezo lakini ingeshinda anaamini Morrison angekuwa habari ya mjini kwa kuzungumziwa zaidi alichokifanya.
“Kama unavyojua michezo ya Simba na Young Africans inavyoongoza kwa mihemko na ndio maana hatajwi Mauya aliyewapa raha wanamtaja mzee Mpili, ila kiuwezo Simba ingeshinda na angefunga Morrison angekuwa habari ya mjini,” amesema Mzee Samatta.
Katika mchezo huo Young Africans walichomoza na ushindi wa bao 1-0, na kufikisha alama 70 kwenye Msimamo wa Ligi Kuu, huku Simba SC ambao ni Mabingwa watetezi wakisalia kileleni kwa kuwa na alama 73.