Kikosi cha Azam FC kimeanza kujipanga kuelekea mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Mabingwa watetezi Simba SC, utakaochezwa juma lijalo jijini Dar es salaam.
Katika mchezo huo wa Ligi Kuu Azam FC watakua wenyeji wa Simba SC katika Uwanja wa Azam Complex Chamazi, na watahitaji kuitumia nafasi ya kucheza nyumbani ili kutimiza lengo la kupata alama tatu muhimu.
Katika kuhakikisha wanaibana Simba SC na ikiwezekana kupata alama tatu siku hiyo, Kikosi cha Azam FC leo kimecheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Pamba FC ya Mwanza iliyoshiriki Ligi Daraja la Kwanza msimu huu 2020/21, katika Uwanja wa Azam Complex Chamazi, Dar es salaam.
Azam FC wamechomoza na ushindi wa mabao 3-0, kwenye mchezo huo. Mabao yakifungwa na Never Tigere, Bruce Kangwa na Ayoub Lyanga dakika ya 25, 31 na 55.
Azam FC inahitaji kulipa kisasi kwa Simba SC, baada ya kukubali kufungwa 1-0 mwishoni mwa mwezi Juni, katika mchezo wa Kombe la Shirikisho (ASFC), uliounguruma Uwanja wa Majimaji mkoani Ruvuma.
Katika mchezo wa Mzunguuko wa kwanza wa Ligi Kuu, timu hizo zilifungana mabao 2-2, Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es salaam.