Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, amezindua Mradi wa Kusambaza Umeme awamu ya pili katika maeneo ya pembezoni mwa jiji la Mwanza (Peri Urban).

Tukio hilo limefanyika, Julai 9, 2021, katika mtaa wa Igogwe, kata ya Chibula, Wilaya ya Ilemela, Mkoani Mwanza.

Akizungumza na wananchi, amesema kuwa Serikali imetoa zaidi ya shilingi Bilioni 9 kuhakikisha kuwa inakwenda kumaliza tatizo la upatikanaji wa huduma ya umeme katika maeneo ya pembezoni mwa jiji hilo.

Amefafanua kuwa, maeneo hayo wamechelewa kupata umeme kwakuwa hayakuwa na sifa ya kupata umeme wa 27,000 lakini kwasababu Serikali ni sikivu imeamua maeneo yote ya mjini yanayofanana na kijijini yapelekewe umeme kwa 27,000.

“ Tulipoanza kusambaza umeme vijijini tukajikuta tumepeleka umeme mwingi vijijini maeneo mengi ya mijini tena yana sura sawa na vijijini hayakuwa na umeme lakini kwasasa kutokana na mradi huu maeneo yote kama haya yatapata umeme wa bei nafuu,”alisema.

Aidha, amemtaka mkandarasi kuhakikisha anasambaza umeme katika maeneo yote ya mitaa hiyo ndani ya miezi 12 ili wananchi wa maeneo hayo waanze mara moja kupata huduma hiyo muhimu.

Ameongeza kuwa, kwakuwa eneo hilo nyumba zipo karibu,hivyo itakuwa rahisi kwa mkandarasi kukamilisha kazi hiyo kwa haraka na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa mkandarasi huyo ili kazi ikamilike mapema.

Amesema kuwa, Taasisi za umma zipewe kipaumbele kuunganishiwa na umeme kwakuwa maeneo hayo ni muhimu katika jamii na bila huduma hiyo hawataweza kutoa huduma bora.

Amesisitiza kuwa, wananchi wakikamilisha malipo ya kupata huduma ya umeme waunganishiwe na huduma hiyo ndani ya siku 14 ili wananchi hao waanza kutumia umeme kwa kujiletea maendeleo mbalimbali.

Vilevile, amemtaka mkandarasi kutumia nguzo za zege kusambazia umeme kwakuwa zinadumu kwa muda mrefu na zitaondoa tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara kwa tatizo la kuanguka kwa nguzo.

Kwa upande wake, Mbunge wa jimbo la Ilemela, Angeline Mabula, ameishukuru Serikali kwa uamuzi wa kuleta mradi wa Peri Urban, kwani umekuwa mkombozi kwa wananchi wa jimbo hilo na kuwataka wananchi kutumia fursa hiyo kwa kuunganisha umeme huo majumbani na kutumia kwa shughuli za kiuchumi.

Nae, Meneja Miradi ya Umeme Vijiji, Kanda ya Ziwa, Mhandisi Ernest Makale, amesema mradi huo mkubwa unatarajia kuunganisha umeme wananchi zaidi ya 10224.

Ameeleza kuwa, uhitaji wa umeme ni mkubwa lakini Serikali imejipanga na itahakikisha kila mwananchi anafikiwa na huduma hiyo.

Dkt. Kalemani, pia amewasha umeme katika zahanati ya Nyamwilolelwa iliyopo katika mtaa wa Nyamwilolelwa, Wilaya ya Ilemela, Mkoani Mwanza.

Manula kuvunja rekodi yake?
Familia 300 za polisi kufaidika makazi ya kisasa