Wanafunzi Watano wa Shule ya Wasichana ya Kiislamu ya AT-TAAUN iliyopo katika Manispaa ya Morogoro, eneo la Mjimpya wamewaishwa Hospitali ya Rufani Mkoa wa Morogoro baada ya kupata mshtuko kutokana na ghorofa mbili za Bweni ya shule hiyo kuwaka moto.
Akizungumza na Dar24Media kwa njia ya simu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro SACP Fortunatus Musilim amesema kuwa, moto huo umetokea majira ya usiku wa kuamkia Julai 11, 2021 ambapo ulianzia gorafa ya pili na kusambaa hadi gorofa ya kwanza panapotumika kama Msikiti.
Aidha Jeshi la Polisi mkoani hapo kwa kushiikiana na Jeshi la Zimamoto pamoja na Shirika la Umeme TANESCO walifanikisha kuwaokoa wanafunzi 102 katika bweni hilo huku watano wakipata mshituko na kupelekwa katika hospitali ya Rufani kwa matibabu zaidi.
Hata Hivyo, TANESCO walifanikisha kukata mifumo ya umeme ili kuzuia madhara yasiendele zaidi, huku chanzo cha moto kikiwa bado hakijajulikana uchunguzi kuendelea.
Kamanda Fortunats amesema kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kutoa elimu kwenye shule za mabweni katika kipindi hiki cha shule kufunguliwa ili kuepukana na ajali za moto mashuleni, lakini pia amewashukuru wananchi kwa kutoa ushirikiano wa karibu kwa kuwa wasikivu na kutokusogea katika eneo la hatari.