”Kupanga ni Kuchagua” ni kati ya maneno pendwa ya aliyekuwa rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati John Magufuli.
Siri iliyo nyuma ya sentensi hiyo pendwa ya hayati Magufuli ni uwepo wa chuo cha mipango hapa nchini kinachofanya tafiti na kuandaa wataalamu katika nyanja mbalimbali kwa lengo kuleta maendeleo vijijini na mijini kupitia wataalamu hao.
Chuo hicho kinachomilikiwa na serikali, kipo chini ya wizara ya fedha na mipango na kina jukumu la kufundisha, kufanya tafiti, na kutoa ushauri elekezi.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1979 chuo cha mipango na maendeleo vijijini kimekuwa chachu ya mabadiliko na kukua kwa sekta mbalimbali kupitia tafiti na ushauri elekezi kutoka kwa wataalamu waliopita katika chuo hiki.
Makamu mkuu wa chuo cha mipango -Taaluma Dkt Provident Dimoso amesema Chuo hicho kitaendelea kutimiza wajibu wake kwa serikali pamoja na jamii nzima ili kuhakikisha nchi inapiga hatua zaidi kimaendeleo na kuwandaa wabobezi wa mipango katika nyanja mbalimbali.
Miongoni mwa taaluma zinazofundishwa na chuo hicho ni mipango ya fedha na uwekezaji, mipango ya maendeleo ya mikoa, mipango ya usimamizi wa rasilimali watu, mipango ya usimamizi wa ardhi, mipango ya idadi ya watu na maendeleo, mipango ya kutengeneza miradi na usimamizi na mipango ya mazingira.