Kiungo kutoka nchini Rwanda Haruna Hakizimana Fadhil Noyonzima amesema anaondoka Young Africans, baada ya mkataba wake kufikia kikomo mwishoni mwa msimu huu, lakini hataacha kucheza soka.
Kiungo huyo ambaye awali alisajiliwa Young Africans mwaka 2011, kabla ya kutimkia Simba SC mwaka 2017, kisha kurejea Jangwani mwaka 2019, ataagwa rasmi kesho Alhamisi ya Julai 15, 2021 kwenye mtanange wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Ihefu SC, dimbani Benjamin Mkapa .
“NAACHANA na Young Africans ila sijaacha soka”. Hiyo ni kauli ya kiungo wa Young Africans Haruna Niyonzima anayetarajiwa kuagwa rasmi klabuni hapo.
“Ninaachana na Young Africans tu! ila bado ni mchezaji, watu wasifikilie kuacha kucheza kwenye klabu hii ndio nimeacha mpira, hapana, mimi bado sana na nina nguvu.
“Kitendo cha uongozi wangu wa Young Africans kuandaa jambo kwa ajili yangu ni heshima kubwa na haitoweza kusahaulika katika maisha yangu ya soka,” amesema Niyonzima.
Niyonzima amesisitiza kuwa kwa sasa anaangalia maisha mengine huenda akaendelea kucheza hapa Tanzania ikitokea timu yoyote inamuhitaji na wakafikia makubaliano.