Uongozi wa klabu ya Juventus ya Italia imekataa kufanya mazungumzo na Klabu ya Chelsea kuhusu uhamisho wa Winga Federico Chiesa.
Chelsea imeonesha nia ya kuhitaji huduma ya winga huyo, na tayari uongozi wa klabu hiyo ya jijini London iliwasilisha ombi la kutaka mazungumzo ili kunogesha mpango wa usajili wa Chiesa.
Juventus imesisitiza kuwa, haiwezi kumuingiza sokoni winga huyo kwa sasa, kutokana na kuhitaji huduma yake kwa udi na uvumba katika kipindi cha msimu ujao wa Ligi Kuu ya Italia.
Juventus ilimsajili kwa mkopo Chiesa akitikea Fiorentina kwa dau la Euro Milioni 10 mwaka 2020, na inatarajiwa kumsajili jumla kwa kulipa Euro Miloni 40.
Chiesa alikuwa sehemu ya kikosi cha Italia kilichotwaa ubingwa wa UEFA EURO 2020, kwa kuichapa England kwa changamoto ya penati jijini London, Jumapili (Julai 11).