Shirikisho la Soka nchini (TFF) limekanusha taarifa za kuwa mbioni kubadilisha Uwanja utakaotumika kwa ajili ya mchezo wa Fainali Kombe la Shirikisho ASFC utakaounguruma Julai 25, kati ya Mabingwa Watetezi Simba SC dhidi ya Young Africans.

Fununu za mabadiliko ya Uwanja, zimeeleza mchezo huo wa Fainali umepangwa kuchezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, badala ya Uwanja wa Lake Tanganyika kwa kigezo cha Uwanja huo kuwa na uwezo mdogo wa kuchukua mashabiki wanaotarajiwa kushuhudia mchezo huo.

Ofisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo, amesema taarifa hizo sio za kweli, na Uwanja wa Lake Tanganyika utaendelea kuwa mwenyeji wa mchezo huo unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka ndani na nje ya Tanzania.

“Hizo ni tetesi tu za kubadilishwa kwa uwanja, mchezo utapigwa hapohapo kama ilivyopangwa awali.” amesema Ndimbo

Kuelekea mchezo huo, Young Africans kupitia kwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano, Injinia Hersi Said, amesema: “Tumejiandaa vizuri kwa ajili ya kuhakikisha tunaibuka na ushindi dhidi ya Simba katika mchezo wetu wa fainali wa Kombe la Shirikisho. Muhimu katika mchezo huu ni kubeba taji hilo. Tunakwenda kwa ajili ya kushinda na si kingine.”

Kesi ya Sabaya mapya yaibuka
Kim Pulsen ataja jeshi la U23