Nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta atatumia jezi namba 15 katika klabu ya Fenerbahce msimu ujao kutokana na jezi namba 10 kukabidhiwa fundi Mesut Ozil.
Mpaka sasa hakuna taarifa zozote kama kulikua na makubaliano kwa wawili hao, zaidi ya picha zilizosambaa mitandaoni zikimuonesha Ozil akiwa amevaa jezi namba 10.
Kama ilivyozoeleka kabla ya kufanywa kwa mabadiliko ya namba ya jezi mwanzoni mwa msimu, huwa kuna makubaliano baina ya wachezaji wenyewe kufuatia ombi la viongozi, lakini kwa waturuki hawa imekua kimya kimya!
Hata hivyo mtandao wa Fenerbahce umeweka wazi juu ya mabadiliko hayo ya namba ya jezi lakini ikitajwa kuwa ni sababu za kibiashara ambapo Fenerbahce watatumia Brand ya “M10” (Mesut Ozil) kwenye mauzo ya jezi na vifaa vingine vya michezo.
Ozil alitua klabuni msimu uliopita akitokea Arsenal ya England, lakini hakubahatika kucheza michezo mingi akiwa na klabu yake hiyo mpya.
Kwa upande wa Samatta aliyekua akicheza klabuni hapo kwa mkopo akitokea Aston Villa ya England, naye amesajiliwa jumla na kwa bahati mbaya amekutana na mabadiliko ya namba ya jezi yake.