Mwenyekiti wa klabu ya Simba Murtaza Mangungu ameshangazwa kwa nini Jina lake halikuwepo kwenye orodha ya viongozi waliojitokeza kuchukua medali wakati Simba wakikabidhiwa kombe la ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara jana Jumapili (Julai 18)..
Mangungu amesema walio na sababu kwa nini yeye hakuitwa kwenda kuchukua medali licha ya kuwepo Uwanjani ni TFF na Bodi ya Ligi kuu Tanzania Bara.
Amesema alitarajia kuwa sehemu ya viongozi wa Simba SC waliotwa kwenda kuchukua medali za ubingwa lakini haikuwa hivyo na ndio maana amewataka TFF na Bodi ya Ligi kutoa sababu.
“Nilikuwepo uwanjani na nilitarajia ningekuwa sehemu ya viongozi waliokwenda kwenye jukwaa la kukabidhiwa medali na kombe la ubingwa,”
“Sikusikia jina langu linatajwa kwenye orodha ya waliokwenda kwenye jukwaa lile, nilishangazwa sana na hilo, lakini wenye mamlaka wanapaswa kuwa na majibu na jambo hili.” amesema Mangungu.
Wachezaji, viongozi wa benchi la ufundi na baadhi ya viongozi wa utendaji wa Simba SC walivishwa medali za Ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2020-21 jana Jumapili (Julai 18), baada ya mchezo wa mzunguuko wa 34 dhidi ya Namungo FC waliokubali kichapo cha mabao 4-0, Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es salaam.