Kocha mkuu wa Simba SC Didier Gomes ameutaka Uongozi wa klabu hiyo kuhakikisha kikosi chake kinaondoka Dar es salaam mapema kuelekea Kigoma, tayari kwa mchezo wa Fainali Kombe la Shirikisho *ASFC*.
Gomes ametoa ushauri huo ili kukiwezesha kikosi chake kupata muda wa zaidi ya siku moja kujiandaa kikiwa mjini Kigoma.
Mratibu wa Simba, Abbas Ali, amesema baada ya mchezo wao na Namungo FC uliochezwa jana Jumapili (Julai 18) watapumzika siku mbili kabla ya Julai 21 kuwahi Kigoma.
Simba SC itaondoka ikiwa ni saa 24 kabla ya Young Africans kuwafuata, kwani imepanga kutua Kigoma Julai 22 baada ya kuwasili Dar es salaam leo Jumatatu (Julai 19) ikitokea Dodoma.
Young Africans ilitinga Fainali Kombe la Shirikisho kwa kuichapa Biashara United Mara bao 1-0, Uwanja wa Alli Hassan Mwinyi, huku Simba SC ikiifunga Azam FC bao 1-0, Uwanja wa Majimaji mjini Songea mkoani Ruvuma.