Mshambuliaji kutoka DR Congo Heritier Ebenezer Makambo, amefunguka kwa mara ya kwanza tangu alipovunja mkataba na klabu ya Horoya AC ya nchini Guinea.
Mapema juma hili, Mshambuliaji huyo wa zamani wa Young Africans aliripotiwa kusitisha mkataba wake, kufuatia changamoto za kukosa nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza.
Jana Jumanne (Julai 20), Makambo alizungumza kupitia kipindi cha michezo cha Clouds FM (Sports Extra) na kusema: “Maisha yalikuwa mazuri tu pale Horoya ila mara baada ya kocha kubadilishwa na kuja kocha mpya ndio shida ilipoanzia, akaanza kuniweka benchi”
“Kwa hiyo kutokana na uwezo wangu kwa kweli nilikuwa naumia sana juu ya kukaa benchi basi nikaamua tu kukaa na kuvunja mkataba kwa maelewano ya pande zote mbili”
“Sababu ya kutoka sio sababu nimepata timu nyingine, ila nime cancel tu kwa maisha maana respect ni kitu muhimu sana kuliko pesa”
“Ofa nilizopokea ni nyingi na siwezi taja timu ambazo zimenifuata, Tanzania ni nchi yangu ya pili maana pale nimeishi kwa raha sana”
“Yanga ni timu yangu naipenda na ikitokea wamehitaji huduma yangu basi nitakwenda na nitapambana kwa kila namna nifanye vizuri zaidi ya kipindi kile”