Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Didier Gomes amesema anatarajia mchezo mgumu dhidi ya Young Africans siku ya Jumapili (Julai 25).
Simba SC ambao ni watetezi wa Ubingwa wa Kombe la Shirikisho watakua na kibarua kigumu cha kubakiza ubingwa huo mikononi mwao dhidi ya watani zao wa jadi, Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma.
Kocha huyo kutoka Ufaransa amesema kikosi chke kipo tayari kwa mpambano huo, lakini hana budi kuwa na mbinu mbadala ambazo zitakuwa shubiri kwa Young Africans siku ya Jumapili.
Amesema anafahamu ladha ya mpambano huo, baada ya kupoteza mchezo wa Ligi Kuu Julai 03, huku akiahidi kuja tofauti.
“Mchezo wa Simba SC na Young Africans siyo mdogo ni mkubwa sana kwani upo katika nafasi ya tano katika dabi bora Africa.”
“Hivyo ni lazima tupate matokeo mazuri ya ushindi utakaokuwa na faida kwangu kutengeneza rekodi na kuwapa furaha mashabiki wetu”
“Tulipoteza mchezo uliopita dhidi ya Young Africans, nimeshafahamu wapi tulikosea, hivyo nimejiandaa vizuri na nitakuwa na mbinu tofauti.”
Gomes alikiongoza kikosi chake kuifunga Azam FC bao 1-0 katika mchezo wa Nusu Fainali Kombe la Shirikisho mjini Songea mkoani Ruvuma mwezi Juni, huku Young Africans wakiifunga Biashara United Mara bao 1-0, mjini Tabora katika Uwanja wa Alli Hassan Mwinyi.