Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Mbaraka Alhaji Batenga amethibitisha kutokea ajali ajali ya moto na kuua watoto wawili wa familia moja katika Kijiji cha Njoro, wilayani Kiteto mkoani Manyara, amesema moto huo uliwaka wakiwa wamelala baada ya kaka yao kuwafungia ndani akaenda kutazama video.
Watoto hao ni Bakari Mursali (8) na Abdi Mursali (6), ambao wakati tukio linatokea wazazi wao hawakupo nyumbani na aliyekabidhiwa jukumu la kuwalea ni kaka yao mwenye umri wa miaka 16, ambaye jina lake halikufahamika.
“Kamati yangu ya ulinzi na usalama tulifika Kijiji cha Njoro saa tano usiku na tukarudi saa 9 usiku tukijaribu kufuatilia sakata hili ambalo hata hivyo uchunguzi unaendelea,” amesema DC Batenga
idha Dc Batenga ametoa elimu ya kukabiliana na majanga ya moto akiwashauri wazazi kuwa makini kutowaacha watoto wakiwa hawana ulinzi, jambo ambalo alisema linaleta madhara kama hayo.
Naye Diwani wa Kata ya Njoro, Ramadhani Mpolonge amesema kuwa wananchi wanashangazwa na tukio hilo kutokana na kwamba nyumba hiyo haipikwi chakula na hakuna chanzo cha moto, huku watoto hao siku hiyo walikula kwa jirani.
“Taarifa za uhakika hawa watoto usiku ule walikula kwa jirani, wakarudi nyumbani kwao na kuingia ndani, ndipo kaka yao akafunga kwa nje na kwenda kuangalia video kwa jirani na aliporudi akakuta moto unawaka ndani,” alisema.