Waziri Ofisi ya Rais (Tamisemi), Ummy Mwalimu amewaahidi Shilingi milioni 5, wachezaji wa Coastal Union, endapo watafanikiwa kubaki Ligi Kuu huku akilipia tiketi za Mashabiki 1,000.
Waziri Ummy ametoa ahadi hizo mbili alipowatembelea kambinj wachezaji wa Coastal Union mapema leo (Jumamosi 24) mjini Tanga.
Waziri Ummy ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini pia amewataka mashabiki wa soka mjini hapo kufika kwa wingi Uwanja wa CCM Mkwakwani kuishangilia timu yao.
Leo saa kumi jioni Coastal Union itacheza mchezo wa mkondo wa pili wa hatua ya mtoano (Play Off) Ligi Kuu dhidi ya Pamba FC ya jijini Mwanza.
Mchezo wa mkondo wa kwanza uliochezwa Jumatano (Julai 21), Uwanja wa Nyamagana Mwanza, timu hizo zilifungana 2-2.
Coastal Union inapambania kubaki Ligi Kuu msimu ujao, huku Pamba FC ikiwania nafasi ya kupanda daraja ikitokea Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara.