Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimezinduwa Ripoti ya Haki za Binadamu na biashara nchini ya mwaka 2020/21 huku kikibainisha uwepo wa changamoto mbalimbali na kutolea mapendekezo ili kuleta maboresho endelevu ya sekta hiyo.
Akizinduwa ripoti hiyo jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu. Bi. Anna Henga (Wakili) alisema ripoti hiyo ni matokeo ya utafiti uliofanywa na LHRC kwa mikoa 15 ya Tanzania Bara, ikihusisha kutembelea maeneo ya kazi na biashara kwa kampuni /mashirika, wanajamii, mamlaka ya udhibiti, na maafisa wa serikali za mitaa.
Wakili Bi. Henga amesema ripoti imeangazia pia haki za binadamu na uchunguzi juu ya maswala yanayohusu biashara na haki za binadamu huku akibainisha vyanzo vya data za ripoti kupatikana kupitia njia anuai zikiwemo vyombo vya habari, kukagua ripoti, sheria, sera, kanuni na hati zingine juu ya sheria za kazi, haki na viwango vinavyotengenezwa na wahusika wa ndani na wa kimataifa.
Aidha alisema ripoti ya 2020/21 imeangazia hali ya haki za Binadamu na biashara ikiwa ni pamoja na hali ya athari za UVIKO-19 katika sekta ya biashara hususani kwenye mikataba ya ajira kati ya wafanyakazi na waajiri, usitishwaji wa ajira usio haki na ulipwaji wa mishahara. Ripoti hiyo pia imeangazia suala la hifadhi za jamii na changamoto zinazohusu wafanyakazi katika michango ya mifuko hiyo ya hifadhi za jamii.
“…Kwa kipekee ripoti imezungumzia haki za wafanyikazi madereva wa mabasi na malori ambao wanakabiliwa na masuala mengi ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kupita kiasi, malipo kidogo, ukosefu wa kandarasi zilizoandikwa au nakala za mikataba, haki ya kuunda na kujiunga na vyama vya wafanyikazi, ukosefu wa mikataba na usalama wa kazi. Utafiti wa ripoti hii umegundua masuala anuwai katika mchakato wa ununuzi wa ardhi kwa madhumuni ya uwekezaji, uwajibikaji wa kijamii na kuheshimu haki za binadamu pamoja na matukio ya uchafuzi wa mazingira kutokana na shughuliza viwanda,”.
Wakili Henga ameongeza kuwa tafiti imebaini Mikataba ya ajira imeshuka ambapo wafanyakazi wengi walioshiriki katika utafiti asilimia 59 walisema wana mikataba ya ajira, huku asilimia 41 wakisema hawana mikataba, ilhali Idadi yawafanyakazi wenye mikataba ya ajira ni pungufu ya asilimia 25 ukilinganisha na idadi ya wafanyakazi wenye mikataba hiyo katika utafiti uliopita wa mwaka 2019, ambapo asilimia 84 walidai kuwa na mikataba ya ajira.
” Ndugu wageni waalikwa; Utafiti huu pia ulibaini obwe kubwa la kukosekana kwa uelewa juu ya sheria za kazi na ajira baina ya wafanyakazi, na hii imepelekea wafanyakazi wengi kutokujua ni wakati gani haki zao zimekuwa zikivunjwa. Mkoa wa Tabora uliongoza kwa k uwa na asilimia kubwa zaidi ya wafanyakazi wasio na uelewa wa kutosha kuhusu sheria na kanuni za kazi (92%). Mikoa mingine ni pamoja na Mbeya (83%), Shinyanga (82%), Mara (81%), Tanga (78%), Dodoma (76%), Singida (73%), Mtwara (72%), na Manyara (71%).
Alizitaja haki za wafanyakazi zilizoripotiwa kukiukwa zaidi kwa ripoti ya mwaka 2020/21 ni; Kutolipwa mishahara, Kucheleweshwa kwa malipo ya mshahara, usitishwaji wa ajira kwa njia isiyo ya haki, punguzo la mshahara lisilo na haki, vitisho vya maneno, udhalilishaji wa maneno, kukataliwa kwa likizo/ kupunguzwa kwa siku za likizo, kufanya kazi saa nyingi bila kupumzika (zaidi ya kawaida na muda wa ziada wa kazi), wafanyakazi kukataliwa kuwa na mikataba/nakala za mikataba hiyo, kutolipwa kwa muda wa ziada, mazingira yasiyo salama ya kazi na pia kukosekana kwa utaratibu wa fidia pale mfanyakazi anapoumia akiwa kazini.
“…tungependa kuiasa serikali kupitia na kuboresha au kubadilisha viwango vya mishahara kwa wafanyakazi wa sekta binafsi kwani Waraka wa Serikali kuhusu Viwango vya Mishahara unaotumika ni wa mwaka 2013. Hata hivyo, waraka huo unatakiwa kupitiwa kila baada ya miaka 3 ili kuboresha mishahara na masharti ya kazi kati ya mwajiri na mwajiriwa. Kuna haja ya kufanyia mapitio waraka huu na kuona namna ya kuboresha mishahara ya wafanyakazi wa kada mbalimbali ili kuwasadia kukidhi gharama za maisha huku tukitambua haki ya kuishi maisha ya hadhi kama mojawapo ya haki muhimu ya binadamu,” alisema Wakili Bi. Henga.
Alisema ripoti hiyo itasambazwa maeneo mbalimbali na kuwataka wadau wote kuisoma na kufanyia kazi mapendekezo kwa ajili ya kuimarisha hali ya haki za binadamu na biashara nchini, na pia kuifanya iwe chachu ya mabadiliko ya hali ya uchumi unaozingatia haki za binadamu nchini.