SIMBA na Yanga wapo kwenye msako wa nyota wapya ili kuimarisha vikosi vyao kwa msimu ujao wa Ligi Kuu, Kombe la ASFC na michuano ya kimataifa ya CAF.
Kutokana na usajili huo maana yake kuna wachezaji huenda wakaonyeshwa mlango wa kutokea na kama kuna watu wana noti zao, wajiandae tu kuwabeba.
Paul Godfrey ‘Boxer’
Amekuwa hapati nafasi ya kucheza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza, licha ya timu hiyo kufanya mabadiliko ya makocha wanne, Luc Eymael, Krimpotic Zlatko, Cedrick Kaze na Nasreddin Nabi.
Boxer amekuwa hapati nafasi ya kucheza mara kwa mara msimu huu na nafasi yake amekuwa akicheza Kibwana Shomary ambaye alisajiliwa msimu uliopita akitokea Mtibwa Sugar.
Yanga imemsajili beki wa kulia kutoka DRC, Djuma Shabani na jambo hilo ni habari mbaya kwa Boxer.
Said Makapu
Tangu ameondoka kocha Eymael katika kikosi cha Yanga, Makapu amekuwa na wakati mgumu wa kupata nafasi ya kucheza kwenye kikosi hicho, licha ya kwamba akipewa nafasi hufunika sana.
Makapu kiasili ni kiungo mkabaji na nafasi hiyo amekuwa akicheza Mukoko Tonombe na muda mwingine hutumika kama beki wa kati ambapo hutumika, Dickson Job, Bakari Mwamnyeto na Lamine Moro, ambaye ameshaagwa Yanga.
Katika dirisha hili la usajili, Makapu amekuwa akihusishwa kujiunga na Mtibwa Sugar na inaelezwa kama ikitokea timu ambayo itampa nafasi ya kucheza anaweza kuondoka Yanga.
Ditram Nchimbi
Tangu amesajiliwa na Yanga akitokea Polisi Tanzania hajawa akipata nafasi ya kucheza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza.
Ugumu ambao Nchimbi anakutana nao katika kikosi hiki licha ya kupata nafasi ya kucheza amekuwa si mzuri katika kufunga licha ya kukutana na nafasi za kufanya hivyo.
Katika msimu huu Nchimbi alifikisha mwaka mzima ndani ya kikosi cha Yanga bila kufunga bao, jambo ambalo linaiweka shakani nafasi yake.
Nafasi ya Nchimbi katika kikosi cha Yanga muda mwingine alikuwa wakitumika, Yacouba Songne ambaye ndio mshambuliaji pekee aliyefanya vizuri msimu huu akiwa kinara kwa kufunga mabao nane.
Tayari inaelezwa Biashara United imeonyesha nia ya kutaka saini ya mshambuliaji huyo mwenye matumizi ya nguvu na kasi.
Ally Salim
Simba wamemuongeza mkataba kipa wao chaguo la tatu msimu huu, lakini nafasi ya kucheza katika kikosi hicho itakuwa ngumu kutokana na Aishi Manula na Beno Kakolanya kutumika zaidi.
Salim si kipa mbaya kwani katika Kombe la Mapinduzi, Kombe la Shirikisho (ASFC), na baadhi ya mechi za kirafiki amekuwa akicheza kwenye kiwango bora.
Simba mbali ya kumsainisha mkataba mpya huenda wakamtoa kwa mkopo ili akapate nafasi ya kucheza katika timu ambazo hazina ushindani na mahitaji kama ya mabingwa hao wa ligi.
Nafasi ya kutumika kwa Salim inaweza kuwa ngumu zaidi kutokana na Simba kumsainisha kipa wa Tanzania Prisons, Jeremia Kisubi ili kuja kuongeza ushindani kwa Manula na Kakolanya.
David Kameta
Beki wa kulia wa Simba, msimu huu amepata nafasi ya kucheza mechi chache za mashindano ya ndani na hakutumika hata katika mchezo mmoja wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ni wazi kumng’oa Shomary Kapombe katika beki ya kulia ni ngumu.
Kameta si mchezaji mbaya kwanza umri wake ni mdogo na alianza kuonyesha ubora huo tangu akiwa katika kikosi cha Lipuli msimu uliopita mpaka Simba kuvutiwa naye na kumsajili.
Ugumu wa Kameta kucheza Simba unaweza kuongezeka zaidi msimu huu kutokana na mabingwa hao wa ASFC, kumsajili beki wa kulia kutokea KMC, Israel Patrick Mwenda.
Miraji Athumani
Winga wa Simba mpaka sasa bado hajafanya mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya na waajiri wake na huenda wasimuongeze mkataba mpya baada ya ule wa awali kufika ukingoni.
Miraji ni moja ya wachezaji wazawa waliokuwa katika kiwango bora ndani ya Simba msimu uliopita akifunga mabao saba katika ligi licha ya kupata nafasi finyu ya kucheza na kuandamwa na majeraha ya mara kwa mara.
Msimu huu Miraji amekuwa akipata wakati mgumu kupenya katika kikosi cha Simba licha ya ubora wake. Nafasi hiyo hutumika zaidi, Luis Miquissone na Clatous Chama.
Wakati Mwingine hucheza Perfect Chikwende au Hassan Dilunga jambo ambalo linaweza kumfanya nyota huyo wa zamani wa Lipuli kutafuta maisha katika klabu nyingine na tayari anahusishwa na Namungo.
Ibrahim Ajibu
Mshambuliaji wa Simba licha ya kuonyesha makali yake akiwa na Yanga misimu miwili iliyopita, huku Msimbazi ameshindwa kufanya mambo makubwa.
Ajibu wakati anarejea katika klabu iliyomlea alitegemewa kufanya mambo makubwa kutokana na uwezo wake wa kufunga mabao, kupiga pasi za mwisho na ufundi mwingine.
Lakini mambo yamekuwa tofauti kwake kwani katika kikosi cha Simba amekuwa mchezaji wa kawaida katika misimu yote miwili na amecheza mechi chache katika mashindano yote. Hivi karibuni aliondoka kikosini kabla ya kumaliza mechi zao za kimashindano. Huenda msimu ujao akatambulishwa kwingineko.