Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi, ameagiza watendaji wa Mahakama mkoani Singida kuharakisha mchakato wa kuandaa eneo litakalotumika kwa mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Manyoni,  itakayaojikita katika kesi za ujangili ili kuimarisha ulinzi wa mazingira.

Profesa Kabudi ametoa agizo hilo wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Singida, alipokutana na viongozi waandamizi wa Mahakama na wadau wa utoaji haki, wakati akikagua hali halisi ya mwenendo wa utoaji haki na utekelezaji wa sheria hususani sheria ya msaada wa huduma za kisheria iliyopitishwa na Bunge mwaka 2017.

“Ujenzi wa mahakama hii ambayo itashughulikia kesi za ujangili, kulinda utajiri wa asili na mali za asili haukwepeki na upo kwenye mpango wa mwaka huu wa fedha,  nataka kufikia Ijumaa muwe mmeainisha eneo la ujenzi wake na mmeshughulikia hati husika nitafika kukagua,” Amesema Profesa Kabudi.

Aidha, Profesa Kabudi amesema dhana na chimbuko la kuanzishwa kwa sheria ya msaada wa huduma za kisheria ni utekelezaji wa takwa la Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Amesema kulingana na Ilani sura 6 ukurasa wa 161 hadi 181 inazungumzia ajenda ya Utawala Bora, Maadili kwenye Utumishi wa Umma, Rushwa, Demokrasia na Haki za Binadamu na kimsingi Wizara ya Katiba na Sheria ndio msimamizi katika kuhakikisha inapanua wigo kwa kuimarisha huduma hizo.

Waziri Kabudi anatarajia kukutana na viongozi na watumishi wote wanaohusika na utoaji haki jinai kwenye wilaya za Ikungi, Iramba, Singida, Mkalama na Manyoni.

Ukichoma chanjo zingatia haya
Dkt Kalemani apiga marufuku kuhamisha nguzo zilizosimikwa