Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki ametoa wito kwa wafugaji wa mifugo ya asili kuunga mkono mkakati wa uboreshaji kosaafu (jamii fulani) za mifugo nchini ili kupata tija zaidi kwa taifa kwa kuwa koo za mifugo zinazopatikana hapa nchini ni nzuri.

Waziri Ndaki amebainisha hayo leo Agosti 3, 2021 jijini Dodoma wakati akizindua mpango mkakati wa uboreshaji kosaafu za mifugo nchini wenye lengo la kuhakikisha kosaafu (jamii fulani) hizo zinazopatikana katika Bara la Afrika na maeneo mengine duniani zinahifadhiwa na kudumishwa kwa ajili ya maendeleo ya nchi na raia wake.

“Ilikuwa lazima mkakati uzinduliwe leo kuhakikisha yale yaliyosemwa kwenye Sera ya Mifugo mwaka 2006, sasa yanakamilishwa kwa sababu tunaweza kuboresha kosaafu ya mifugo lakini hatukuwa na mikakati ya namna sera hiyo inaweza kuboresha kosaafu ya mifugo yetu ya asili.” Amesema Waziri Ndaki.

Aidha Waziri Ndaki amesema kuwa nchini kuna mifugo ya aina nyingi na hizo zote ni kosaafu za mifugo ambazo zinatakiwa kulindwa kuhifadhiwa na kuendelezwa kwa njia ya ubora zaidi ili kunufaisha watu wake hivyo mkakati huo utasaidia kuona namna gani ya kuboresha ili ziweze kuwanufaisha zaidi wafugaji.

Kwa upande wake Mratibu wa Kosaafu za Mifugo hapa nchini kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Hassan Mruttu amesema tayari kulishakuwa na rasimu na kuanza utekelezaji kwa ufadhili wa Shirika la Umoja wa Afrika la Rasilimali za Mifugo (AU-IBAR) kwa kuanzisha kikundi cha wafugaji wa mbuzi weupe wa kipare na kuwezesha kupata mbegu ya ng’ombe aina ya sahiwal ambayo inakuwa na nyama na maziwa mengi pamoja na kusaidia uhifadhi wa mbegu hizo.

Akizungumza kuhusu mkakati huo mmoja wa wafugaji wa ng’ombe wa asili Elinami Mshao amesema matarajio yao ni kupata faida kwa kupata mbegu bora za mifugo na kwa bei nafuu ambapo serikali itawafikishia kwa kuwa baadhi ya aina ya ng’ombe wakiwemo waliopo nchini jirani wanauzwa bei ghali na wamekuwa na matokeo mazuri kwa wafugaji.

Ameongeza kuwa wao kama wafugaji uchumi wao mkubwa unategemea mifugo hivyo ikiboreshwa itakuwa na tija kwao kwa kuwa watapata mbegu bora ya mifugo ya asili.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akizindua Mpango Mkakati wa Uboreshaji Kosaafu za Mifugo nchini, katika hafla fupi iliyofanyika jijini Dodoma na kutaka mpango huo uwawezeshe wafugaji wa asili kuboresha mifugo yao na iwe na tija zaidi kwa taifa
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza na washiriki wakati wa uzinduzi wa Mpango Mkakati wa Uboreshaji Kosaafu za Mifugo nchini, katika hafla fupi iliyofanyika jijini Dodoma na kubainisha kuwa kosaafu za mifugo zilizopo nchini ni nzuri hivyo zinapaswa kuboreshwa ili zitoe matokeo mazuri zaidi.
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) ambaye pia ni Msajili wa Baraza la Veterinari Tanzania Dkt. Bedan Masuruli akifafanua jambo wakati wa uzinduzi wa Mpango Mkakati wa Uboreshaji Kosaafu za Mifugo nchini, katika hafla fupi iliyofanyika jijini Dodoma.
Mratibu wa Kosaafu za Mifugo nchini kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Hassan Mruttu, akifafanua namna wizara itakavyohakikisha inatekeleza yale yote yaliyopo kwenye Mpango Mkakati wa Uboreshaji Kosaafu za Mifugo nchini, katika hafla fupi iliyofanyika jijini Dodoma.

EWURA imesitisha bei ya gesi ya kupikia
Kamati yaundwa kuchunguza moto Msamvu