Taarifa zinasema kuwa Benchi la Ufundi la Mabingwa wa Soka Tanzania Bara, Simba SC limeagiza wachezaji kurejea kambini leo Jumapili (Agosti 08), tayari kuanza maandalizi ya msimu mpya wa 2021/22.
Agizo hilo limetolewa na Kocha Mkuu Didier Gomes, huku akisistiza wachezaji wa zamani na wale wapya watakapofika kambini wafanyiwe vipimo kama ilivyo kawaida kabla ya msimu kuanza.
Mara baada ya zoezi hilo la vipimo, Agosti 11 na 12, wachezaji wote watapatiwa jezi mpya za msimu ujao watakazozitumia katika mazoezi, mechi pamoja na sare watakazokuwa nazo kwenye shughuli nyingine.
Baada ya hapo siku moja mbele watakwea pepa na kwenda Morocco kuweka kambi ya wiki zisizopungua mbili itakayoambatana na mechi za kirafiki tayari kwa msimu mpya wa Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika unaotarajiwa kuanza mwezi ujao.