Kiungo Jonas Gerrard Mkude ni sehemu ya wachezaji wa Simba SC walioripoti Kambini mapema leo Jumatatu (Agosti 09), tayari kwa kuanza maandalizi ya Kambi kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na Michuano ya Kimataifa.
Hii ni mara ya kwanza kwa kiungo huyo kuonekana akiwa na wachezaji wenzake wa Simba SC, baada ya kusimamishwa kwa sababu za utovu wa nidhamu.
Mkude ameonekana mwenye furaha baada ya kukutana na baadhi ya wachezaji wenzake wa Simba SC, huku wengine wakitarajiwa kuwasili kambini hapo baadae hii leo.
Simba SC imepanga kuweka kambi nchini Morocco kwa maandalizi ya msimu mpya wa 2021/22, ambao utaanza rasmi mwezi ujao.
Kabla ya kuanza kwa msimu mpya, Simba SC itacheza michezo ya kirafiki ikiwa ni sehemu ya kuajiandaa na mkakati wa kutetea mataji la Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho na kufika mbali katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Msimu uliopita Simba SC ilifika hatua ya Robo Fainali na kutolewa na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini kwa kufungwa jumla ya mabao 4 kwa 3.