Wapiganaji wa kundi la Taliban wamefanikiwa kushika majiji mengine matatu makubwa nchini Afghanistan ya Kunduz, Sar-i-Pul and Taliqan kufuatia mapigano makali yaliyotokea jana dhidi ya majeshi ya Serikali.

Taarifa kutoka Afghanistan zinaeleza kuwa hatua hiyo imefanya majiji matano makubwa kukamatwa na wapiganaji wa Taliban ndani ya wiki moja, kundi ambalo awali liliingia makubaliano maalum na Marekani kusitisha mashambulizi katika majiji muhimu.

Hatua hiyo inakuja wakati Rais wa Marekani, Joe Biden ameahidi kuendelea na mpango wa kuyaondoa majeshi ya Marekani kwenye ardhi ya Afghanistan, na hadi sasa ameahidi kutobadili uamuzi wake.

Tangu Marekani ianze kuyaondoa majeshi yale, kundi la Taliban limeongeza nguvu na kukamata zaidi ya nusu ya wilaya 400 za Afghanistan.

Msemaji wa Taliban aliiambia Al Jazeera jana kuwa hakuna makubaliano yoyote kati ya kundi hilo na Serikali ya Afghanistan kusitisha mapigano. Pia, alionya hatua za Marekani kuingilia tena mambo ya nchi hiyo.

Taliban ndilo kundi lililokuwa likiiongoza Serikali ya Afghanistan kwa sheria za dini chini ya kamanda wake, Mullah Mohammed Omar. Kundi hili lilikuwa na maelewano ya kawaida na Marekani hadi pale walipokuwa wamemuhifadhi Osama Bin Laden (aliyekuwa kiongozi wa Al-Qaeda) na kukataa kumkabidhi kwa majeshi ya Marekani baada ya tukio la kigaidi la Septemba 11, 2001.

Mullah aliamua kukubali kupigwa na Marekani kuliko kuwapatia Osama Bin Laden, rafiki yake aliyekuwa amemhifadhi. Alisema dini hairuhusu kumkadbidi kwa adui mtu aliyeomba hifadhikwako.

Baada ya operesheni ya kumsaka Osama Afghanistan, Marekani iliwaondoa Taliban madarakani na wakawa wapiganaji walioishi milimani na wakapewa kofia ya ugaidi. Mullah alifariki mwaka 2013 baada ya kutafutwa sana na Marekani bila mafanikio.

Hivyo, kwa miaka 20 sasa, Taliban wanapigana na Serikali ya Afghanistan wakitaka kurejea madarakani.

Hatua hii inaifanya Marekani kuendelea kukuna kichwa kufuatia uamuzi wake kutaka kuondoa majeshi yake yote nchini humo, kwani kuna dalili kuwa ndani ya kipindi kifupi Serikali ya Afghanistan inaweza kurejea mikononi mwa Taliban.

Mbaroni kwa kumuozesha mtoto
Mkude arudi Simba SC kwa kicheko