Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir ameagiza kusitishwa mara moja kwa mapigano ya ndani yaliyopo kati ya makundi mawili ya kijeshi, moja likiongozwa na Rais na jingine likiongozwa na makamu wake.
Rais Kiir amesema kuwa kundi hilo linaloongozwa na mpinzani wake wa zamani ambaye ni Makamu wa Rais Riek Machar lilisababisha machafuko ya mwishoni mwa wiki na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 30.
Wito wa Kiir umekuja wakati Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Mashariki mwa Afrika – IGAD ikionya kuwa kuvunjika kwa vuguvugu la Machar la Sudan People’s Liberation Movement/Army-In Opposition – SPLA-IO ni zaidi ya mgogoro wa ndani ya chama na unaweza kusababisha athari kubwa za sasa na siku za usoni kwa taifa hilo changa ulimwenguni.
Ofisi ya Kiir imetoa taarifa ikitaka kusitishwa kwa uhasama kati ya kambi hizo mbili. Mkutano wa dharura wa mawaziri wa mambo ya kigeni wa IGAD umezitaka pande kuanza mazungumzo ya amani.