Beki kutoka DR Congo Henoc Inonga Baka ‘Varane’ anatarajiwa kusafiri leo Alhamis kuelekea mjini Casablanca nchini Morocco, kwa ajili ya kujiunga na wachezaji wa Simba SC walioweka kambi nchini humo.
‘Varane’ jana alifika Hospitali ya taifa ya Muhimbili akiwa na wachezaji wengine wa Simba, Chris Mugalu, Ally Salim, Said Ndemla, Ibrahim Ajib, Yusuph Mhilu pamoja na mratibu wa timu hiyo Abas Suleiman kwenye walipokwenda kupata chanjo ya Covid -19.
Henoc alifika Hospitali hapo mishale ya saa 7:00, akiwa amevaa pensi na tisheti za kijani iliyokolea sana, kofia nyeusi na raba kali iliyochanganya rangi akiongozana na Mkongomani mwenzake Mugalu sambamba na Abas, Mhilu na Ally na kulekea katika kitengo cha Jakaya Kikwete Cardiac Institute (JKCI) ambapo chanjo ya Covid -19 inatolewa.
Kitasa hicho (‘Varane’), kimesajiliwa na Mabingwa wa Soka Tanzania Bara katika kipindi hiki cha dirisha la usajili kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Michuano ya Kimataifa, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kukiboresha kikosi cha Simba SC.