Mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba SC, wamethibitisha taarifa za kuuzwa kwa kiungo kutoka nchini Zambia Clatous Chotta Chama, kwenye klabu ya RS Berkane ya Morocco.
Taarifa za kuuzwa kwa Chama zilipokelewa kama tetesi tangu jana Alhamis (Agosti 12) majira ya usiku, huku picha ya kiungo huyo ikisambaa akionekana akiwa kwenye mazoezi ya kikosi cha RS Berkane ya Morocco.
Kaimu Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Simba SC Ezekiel Kamwaga, amethibitisha taarifa za kuuzwa kwa chama leo Ijumaa (Agosti 13) asubuhi.
“Ni kweli tumemuuza Chama, pesa tuliyomuuza ni kubwa zaidi ukilinganisha na pesa tuliyomnunulia, pesa aliyouzwa chama itatumika kuboreshea kikosi cha Simba lakini pia tumeangalia maslai ya mchezaji na klabu.
Mashabiki wa Simba wasiwe na wasiwasi kwani waliomleta chama ndio watamleta mbadala wake.
Kuhusu Miquissone bado ni mchezaji wetu, ameomba ruhusa ili ashughulikie mambo yake binafsi na atakaporudi tutawapa taarifa kama tutaendelea kuwa nae au ataondoka” alisema Kamwaga
Taarifa zinaeleza kuwa Chama ameuzwa kwa ada ya Shilingi Bilioni 1.5, na sasa atacheza sambamba na kiungo kutoka DR Congo Tuisila Kisinda anaedaiwa kutua RS Berkane akitokea Young Africans.
Hitaji la Chama kwenye klabu hiyo lilinogeshwa na uwepo wa Kocha Florent Ibenge aliyeukubali uwezo wa kiungo huyo, pindi alipokua mkuu wa benchi la ufundi la AS Vita Club.
Awali Chama alikuwa akiwaniwa na klabu ya FAR Rabatt ya Morocco, inayonolewa na aliyekuwa kocha wa Simba SC Sven Vanderbroek.