Aliyekuwa Mchezaji na Kocha wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Abdallah King Kibadeni, amesema Uongozi wa klabu hiyo hauna jeuri ya kukataa ofa zinazotumwa kwa sasa.
Simba SC imekuwa sehemu ya klabu za soka Barani Afrika zinazohusishwa na taarifa ya baadhi ya wachezaji kutakiwa na klabu za kaskazini mwa Afrika.
Kibadeni amesema Simba SC kwa sasa haijafikia hatua ya kukataa ofa za wachezaji, zinazotumwa kutoka Afrika Kaskazini kwa sababu zinaambatana na pesa nyingi sana.
Amesema klabu hizo zimejipanga kifedha na zina uwezo mkubwa, hivyo lolote wanalolidhamiria wana asilimia kubwa ya kufanikiwa hasa kwa klabu za ukanda wa Afrika Mashariki.
“Hatuwezi kushindana na timu kama Al Ahly na wengineo, timu zetu bado zina uwezo mdogo wa kifedha kushidana na timu za Kaskazini hivyo pesa ambayo imetajwa kwa wachezaji hao ni vigumu sana kwa kiongozi yeyote wa klabu kuikataa.”
Tayari Simba SC imekubali kumuachia kiungo kutoka Zambia Clatous Chotta Chama kwa dau linalotajwa kufikia Shilingi Bilioni 1.5, huku Miquissone akihusishwa na taarifa za kunyatiwa na mabingwa wa Afrika Al Ahly ya Misri.