Watu 304 wamepoteza maisha nchini Haiti baada ya kutokea tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa magnitude 7.2 lililoangusha majengo kadhaa.
Mkuu wa Wakala wa Usalama wa Raia, Jerry Chandler amethibitisha idadi hiyo ya vifo kupitia taarifa aliyoitoa jana, akieleza kuwa takribani watu 1,800 wamejeruhiwa na wengine wameyakimbia makazi yao.
Chandler amefafanua kuwa watu 160 walifariki Kusini; 42 walifariki Nippes; 100 walifariki Grand Anse; na wawili waliripotiwa kupoteza maisha wakiwa Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo.
“Msaada wa haraka uliotolewa na wataalam wa uokoaji pamoja na wananchi kwa ujumla ulisaidia kuwaokoa watu wengi ambao walikuwa hatarini. Hospitali zinaendelea kupokea majeruhi na wanafanya kazi kubwa,” alisema kupitia Twitter.
Tukio hilo lilitokea Jumamosi, Agosti 14, 2021 majira ya asubuhi.
Waziri Mkuu wa Haiti, Ariel Henry ametangaza mwezi mmoja wa hali ya dharura, akieleza kupitia Twitter kuwa Serikali itatumia rasilimali zake kadiri iwezekanavyo kukabiliana na tatizo hilo na kuwasaidia wahanga.