Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo amewaagiza watumishi wa Kikosi cha Jeshi la Polisi cha Kupambana na Dawa za Kulevya visiwani Zanzibar kuongeza kasi kwenye doria ya uhalifu wa dawa za kulevya ili kukamata watuhumiwa Zaidi na kunusuru nguvu kazi ya taifa ambao wanaathirika na madawa hayo.
Ameyasema hayo leo Agosti 15, 2021 wakati wa kikao na Jeshi hilo cha mkakati wa kupambana na uhalifu wa Dawa za Kulevya huku jamii ikiaswa kutambua dawa za kulevya ni uhalifu kama uhalifu mwingine.
“Hali ya uhalifu wa dawa za kulevya huko mtaani ni mbaya, vijana wanaaribika,uhalifu unaochochewa na dawa za kulevya ni mkubwa sana, nawaombeni mzidishe misako,doria ili kunusuru nguvu kazi ya taifa hili,viongozi wetu wanawategemea vijana katika kukuza uchumi wa nchi hii, shirikianeni na jamii pelekeni elimu kwenye jamii kwani jamii inachukulia dawa za kulevya kama sio uhalifu tofauti na aina nyingine za uhalifu,” Amesema Naibu Waziri Chilo.
Akisoma taarifa za Takwimu Mkuu wa Kikosi cha Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Omar Khamis amesema kuwa Jumla ya Kesi 678 za Dawa za Kulevya zimekamatwa na Jeshi hilo katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2018 mpaka Agosti mwaka 2021.
“Mheshimiwa kitengo kimefanikiwa katika ukamataji wa kesi ambapo mwaka 2017 jumla ya kesi 213 zilikamatwa,mwaka 2018 kesi 183,mwaka 2019 kesi 131,mwaka 2020 kesi 93 na hadi kufikia mwezi Agosti mwaka huu kesi 58 zilikamatwa katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar ambapo tayari washtakiwa tayari washaanza kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria namba 9 ya mwaka 2009 ya kudhibiti dawa za kulevya,” Amesema ACP Omar.
Kwa kipindi cha mwezi januari hadi sasa Jeshi la Polisi limefanya operesheni mbalimbali za kupambana na uhalifu ikiwemo ukamataji wa dawa za kulevya huku heroine zenye uzito wa kilogramu 1 na gramu 287.51 zikishikiliwa na bangi kilogramu 120 na gramu 651.984 zikishikiliwa.