Beki wa pembeni wa Young Africans Paul Godfrey ‘Boxer’ amemtangazia vita kiungo wa pembeni kutoka DR Congo Jesus Moloko.
Moloko aliyekuwa AS Vita Club, amesajiliwa Young Africans kuchukua nafasi ya Tuisila Kisinda aliyetimkia RS Berkane ya Morocco.
Boxer anaamini anaweza kucheza kama kiungo wa kulia tofauti na nafasi ya beki wa upande huo, hivyo amemtaka Moloko ajiandae kupambania namba kwenye kikosi cha kwanza.
Beki huyo mzawa amesema baada ya kukosa nafasi msimu uliopita kufuatia uwepo wa Kibwana Shomari, amejifunza mambo mengi, na anaamini nafasi ya kiungo wa kulia itamfaa.
Boxer amesema: “Ukiangalia kule kulia wakati yuko Kibwana tu sikupata sana nafasi ya kucheza lakini sasa tunakuwa watatu baada ya Djuma kuja hakuna namna naona kutakuwa na ugumu wa kuwania nafasi kitu ambacho naweza kuja kuwa chaguo la tatu kwa kocha,
.
“Unajua hii nafasi ya beki wa kulia haikuwa nafasi yangu nilikuwa nacheza winga ya kulia lakini wakati ule kocha Zahera akaniomba nirudi kucheza nyuma baada ya kaka yangu Juma (Abdul) kuumia nafikiri sasa ni wakati wangu kurudi katika nafasi ileile nishindane na huyu Moloko,”
“Kama (Moloko) ana kasi hata mimi nina kasi,kitu kizuri sasa nimeimarika zaidi naweza pia kurudi kuja kukaba kwa nguvu nikitumia uzoefu wa kucheza kama beki wa kulia,nitaongea na kocha kumuomba hili mara tu tutakapoanza maandalizi ya huku Morocco akikubali watu watamuona Boxer mpya msimu ujao.” amesema Paul Godfrey Boxer
Chanzo: Mwananchi